RUVU SHOOTING YAZIDI KUJIFUA KUELEKEA MSIMU MPYA WA LIGI KUU

Na Zainab Nyamka,Globu ya Jamii

LICHA ya baadhi ya timu kutoanza mazoezi kipindi hiki cha mwezi mtukufu wa Ramadhani, timu ya Ruvu Shooting imeendelea kujifua kuelekea msimu ujao wa Ligi Kuu Tanzania Bara baada ya kupanda tena  daraja msimu huu ikiongoza kundi B  na kuingia kambini mapema hata kabla ya kumalizika kwa Ligi Kuu.

Afisa habari wa timu hiyo, Masau Bwire amesema kuwa timu yao  inaendelea na mazoezi licha ya kuendelea kwa mwezi wa ramadhani, msimu ujao ni muhimu sana kwao kwani wanataka kudhihirisha kuwa walifanyiwa hujuma za kushushwa daraja msimu wa 2014/15.

Masau alisema kuwa timu yao bado inakikosi bora ndio maana wamefaniiwa kirudi Ligi kuu wakiwa na alama ambazo hazikuweza kufikiwa na timu yoyote ndani ya kundi lao. "Tunajua kuwa mfungo wa mwezi mtukufu wa ramadhani ni ibada muhimu lakini pia haiwazuii wachezaji kufanya mazoezi au kazi nyingine ambazo ni muhimu kwao", amesema Masau.

Amesema kuwa kuelekea msimu ujao wa ligi kuu mwalimu wa timu hiyo, Tom Olaba anataka kufanya mabadiliko ya kikosi chake kwa kukiongezea nguvu katika baadhi ya maeneo kwani mapendekezo yake  ni kuongeza wachezaji saba wa nafasi mbalimbali na alishapeleka suala hilo kwa uongozi.

Masau amesema kuwa timu hiyo itafanya usajili kutokana na mapendekezo ya mwalimu huyo ambayo yataungwa mkono kwa asilimia mia moja.

Maoni