"UKAE juu ya kiti. Ili uandike hati, ndogo ya husia. Mimi kwako ni baba. Hati hii ya huba. Andika iwe akiba. Hasa itakufaa. Aliwahi kuandika mwalimu wa lugha ya Kiswahili hayati Shaaban Robert katika moja ya kitabu chake cha utenzi wa hati.
Robert anabaki kuwa kati ya waandishi mahiri sana katika kutumia lugha ya Kiswahili duniani. Kipaji chake katika hilo ndio kimemfanya aonekane nguli kila mahali. Hakika Shaaban Robert ni nguli wa lugha adhimu ya kiswahili duniani. Tuachane na hilo.
Liverpool imetaabika katika kupata kiungo mkabaji wa kuimarika kwa kipindi kirefu tangu walipoondoka viungo Xabi Alonso na Javier Mascherano, ambao walitimkia Real Madrid na FC Barcelona. Hakika Mascherano na Alonso walikuwa roho ya Liverpool kwa miaka ile.
Unakumbuka kile kilichotokea Instambul, Uturuki mwaka 2005? Hadi mapumziko AC Milan ilikuwa inaongoza mabao 3-0. Kilichotokea katika kipindi cha pili ni kama yale maajabu yaliyofanywa na nabii Mussa kunyooshea fimbo katika bahari. Hakika bahari ilifunuka na kuweka njia kati.
Ni sawa na yale maajabu yaliyofanywa na FC Barcelona dhidi ya PSG katika hatua ya mtoano ya ligi ya mabingwa Ulaya mapema mwaka huu. Hakika wachache ndi waliotabiri Come Back ile ya ajabu.
Tuwaacheni mashabiki wa Liverpool waendelee kuipenda timu yao tu. Tuwaacheni haina jinsi. Kwa mpira ule uliopigwa pale Instanbul hakuna shabiki anayeweza kuitosa Liverpool.
Katika kufanya vibaya kwa Liverpool miaka ya hivi karibuni hususani kutoshiriki katika michuano ya klabu bingwa Ulaya miaka kadhaa, imetokana na kukosa kikosi imara ikiwemo kiungo mkabaji. Na sio kiungo mkabaji bali kiungo mkabaji halisi. Man to man na Box to Box midfilder.
Tukiachana na Jordan Henderson ambaye ni mzuri zaidi katika nafasi ya kiungo namba nane, kulikuwa na Lucas Leiva ambaye ni mkabaji mzuri aliyekuwa na mazoea ya kuipoozesha timu pamoja na kuanza mashambulizi. Si kiongozi wa viungo wenzake. Hiyo ndio ilikuwa sababu ya Liverpool kufanya vibaya katika miaka ya hivi karibuni.
Msimu uliopita walimpata Giorgino Wiljnadum. Hakika ni moja ya viungo bora kwa sasa. Lakini naye sio mzuri katika kukaba. Anafahamu kukaba lakini sio wa kukaa nyuma kwa ajili ya kusaidia akina Lovren. Giorgiono ni mzuri zaidi kukabia juu. Hakika anahitaji box to box ili afurahie dimba la pale Anfield.
Liverpool ilikosa kiungo kiongozi. Mkongwe Steven Gerrard alikuwa kiongozi. Pia, Alonso na Mascherano walikuwa viongozi. Kwa nini Liverpool ya sasa inakosa kiungo kiongozi wa kuwamiliki wenzake dimbani?
Hakuna timu inayotwaa ubingwa wa ligi kuu England au ligi ya mabingwa Ulaya bila ya kuwa na kiungo kiongozi. Kulikuwa na Patrick vieira, Roy Keane, Yaya Toure, Paul Scholes na wengineo hao ni wachache tu.
Liverpool inahitaji kiongozi wa kati, inahitaji mshindi wa mipira ya kati yaani 'ball winner', mshindaji wa mipira yote ya chini na juu ya uwanja. Inahitaji kiungo anayefanya kazi kupita kiasi, mtu wa kucheza pasi za haraka baada ya kukaba.
Katika moja ya maandiko ya Hayden Ferry, mchezaji wa mpira wa miguu nchini Marekani aliwahi kusema kuwa mpira ni sawa na maisha.
"Hakika soka ni sawa na maisha, lazima ujifunze kucheza kutokana na kanuni zake zinavyosema." Hakika Liverpool inahitaji kiungo mahiri atakayecheza kutokana na kanuni za ukabaji.
Siku za hivi karibuni katika kulijua hilo, kocha wa Liverpool Jurgen Klopp ameamua kutumia nguvu kuishawishi klabu yake kumsajili kiungo wa timu ya RB Leipzig, Naby Keita. Hakika Klopp hajawahi kubahatisha katika kiungo mkabaji wa uhakika.
Tuliwahi kushuhudia kwa Sven Bender na Jakub Blaszczykowski. Wachezaji hawa hawakuwa na masihara kabisa. Mnaikumbuka Borussia Dortmund iliyoifunga 4-0 Real Madrid? Madrid ilikula hizo na kutolewa kwa tofauti ya mabao katika ligi ya mabingwa Ulaya.
Na kile kilio cha Dortmund katika fainali baada ya kufungwa na Bayern Munich kilikuwa sahihi kabisa. Acha Klopp aendelee kummezea mate Keita. Acha Keita aendelee kuwa na ndoto za kucheza Livepool. Keita anapenda kucheza Liverpool anahitajika hata leo hii.
Kiburi cha Mwenyekiti wa Leipzig, Oliver Mitzlaff kinaendelea kumuumiza Keita. Kocha wa Leipzig, Ralph Hasenhuttl alishakubali mapema kuwa moyo wa Keita umehamia upande wa Liverpool, lakini Mitzlaff anaendelea kumdengulia mwenyekiti makini wa Liverpool, Tom Werner.
Kugomea mazoezi, kumchezea rafu mbaya mchezaji mwenzake katika mazoezi ni baadhi ya matokeo yanayoonyesha Keita anahitaji kuwa wa Liverpool si wa Leipzig tena.
Matukio ya Keita yanaonyesha moyo wake upo kwa Klopp na mwili wake pekee ndio wa Leipzig. Inahitaji mkabaji halisi, Keita ni suluhisho hilo. Ana uwezo wa kufunga ni kiongozi wa wenzake na anapiga pasi za uhakika. Hakika Keita ni dawa ya Klopp pale Liverpool. Lazima tukubali hilo. Bila ya kupepesa macho. Naweza kusema hadi sasa Liverpool haina kiungo wa kucheza 'box to box’ mwenye haiba kama ya Keita. Klopp anataka saini ya Keita kwa sababu anahitaji ulinzi kwa mabeki na wakati huo huo anahitaji washambuliaji wapumzike.
Anahitaji Sadio Mane, Philippe Coutinho, Mohamed Salah na Firmino wasiwe na mzigo mkubwa wa kukaba. Keita huenda akaongeza nguvu ya Liverpool kupigania taji la EPL kwa nguvu zote, kwani majogoo hao wa Anfield watahitaji kikosi kipana cha kuanza mapambano kwa kujiamini.
Keita ataisaidi Liverpool. Klopp hajawahi kubahatisha katika kumsajili mchezaji mkabaji. Keita ana kila sababu za kuwa chaguo la kocha huyo Mjerumani.
Kuwa na kiungo kama Keita kwa sasa ni muhimu kwa timu yoyote. Keita hana utofauti na Granit Xhaka, N'Golo Kante na Carlos Casemiro. Hakika hawa ndio viungo wanaotakiwa kwa sasa katika ulimwengu wa soka.
Keita ana kazi saba za kiungo yeyote mkabaji bora ambazo lazima awe nazo. Kwanza anakaba, analinda mabeki wake, ni mzuri katika mipira ya kulala kuhakikisha anazuia hatari langoni kwake. Keita ana uwezo wa kuwadhibiti viungo wa timu pinzani, ni mzuri katika kupiga pasi za haraka baada ya kukaba.
Pia, ni kiongozi wa wenzake, hakika ana kila sababu za kuisaidia Liverpool. Tuendelee kuona filamu hii ya Keita na kiburi cha mwenyekiti wa Leipzig inavyoendelea kushika hatamu.
|
Maoni
Chapisha Maoni