Mkuu
wa Mkoa wa Simiyu, Mhe.Anthony Mtaka akizungumza na Viongozi na Askari wa Jeshi
la Polisi wa Mkoa huo (hawapo pichani) katika kikao kilichofanyika Mjini Bariadi.
Baadhi
ya Askari Polisi wakimsikiliza Mkuu wa Mkoa wa Simiyu Mhe.Anthony Mtaka(hayupo
pichani) katika kikao kilichofanyika Mjini Bariadi.
Kamanda
wa Polisi wa Mkoa wa Simiyu, Boniventure Mshongi akizungumza katika kikao cha
Viongozi na Askari wa Jeshi la Polisi na Mkuu wa Mkoa wa Simiyu kilichofanyika
Mjini Bariadi.
Baadhi
ya Viongozi wa Jeshi la Polisi wakimsikiliza Mkuu wa Mkoa wa Simiyu Mhe.Anthony
Mtaka(hayupo pichani) katika kikao kilichofanyika Mjini Bariadi.
Baadhi
ya Askari Polisi wakiimba Wimbo wa Maadili mbele ya Mkuu wa Mkoa wa Simiyu
Mhe.Anthony Mtaka(hayupo pichani) kabla ya kikao kilichofanyika Mjini Bariadi.
Baadhi
ya Viongozi wa Jeshi la Polisi wakiimba wimbo wa Maadili ya Polisi mbele
ya Mkuu wa Mkoa wa Simiyu Mhe.Anthony
Mtaka(hayupo pichani) kabla ya kikao kilichofanyika Mjini Bariadi.
WP
Anna akichangia jambo katika kikao cha Mkuu wa Mkoa huo na Viongozi na Askari
Polisi kilichofanyika leo Mjini Bariadi.
PC
Simon kutoka Wilayani Busega akichangia
jambo katika kikao cha Mkuu wa Mkoa huo na Viongozi na Askari Polisi
kilichofanyika leo Mjini Bariadi.
Mkuu
wa Mkoa wa Simiyu, Mhe.Anthony Mtaka akizungumza na Viongozi wa Jeshi la Polisi
wa Mkoa huo ( baadhi hawapo pichani) kabla ya kikao kilichofanyika Mjini
Bariadi.
Na Stella Kalinga, Simiyu
Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe.Anthony Mtaka amelipongeza Jeshi la Polisi Mkoani humo kwa
kupunguza matukio ya uhalifu hali iliyobadili taswira ya mkoa na kuufanya usikike
katika masuala maendeleo.
Mtaka ametoa pongezi hizo katika kikao chake na
Viongozi na Askari wa Jeshi la Polisi Mkoani humo kilichofanyika leo Mjini Bariadi.
Amesema askari wa Jeshi la Polisi wamefanya kazi
kubwa katika kubadili taswira ya mkoa wa Simiyu ambapo kwa sasa viongozi na wananchi
wamekuwa wakijadili masuala ya maendeleo ukiwemo Uchumi wa Viwanda kwa sababu
ya amani na utulivu uliopo.
“Simiyu ya zamani ni tofauti kabisa na ya sasa, zamani tulikuwa tukiangalia TV, tukisikiliza
redio au kusoma magazeti habari zilikuwa ni mauaji ya vikongwe, kukatana
mapanga na mauaji ya watu wenye ualbino.
Pamoja na viongozi wa Dini kuomba Mungu kwa ajili ya mkoa wetu lakini
Jeshi la polisi pia limefanya kazi kwa nafasi yake pamoja na vyombo vya Ulinzi
na Usalama ” alisema Mtaka.
Aidha,
amesema Serikali imedhamiria kuujenga Mkoa wa Simiyu kuwa Mkoa mpya wa kiuchumi
jambo ambalo linapaswa kujulikana na wadau wote muhimu wa maendeleo wakiwemo
viongozi na askari wa Jeshi la Polisi ambao aliwataka kuchangamkia fursa
mbalimbali za uwekezaji na maendeleo mkoani humo.
“ Chini ya Falsafa ya Wilaya Moja Bidhaa Moja, Sasa
hivi Maswa wanatengeneza chaki, Meatu wanasindika Maziwa na tunapanua kiwanda
cha maziwa kwa kufanya uwekezaji mkubwa ambapo pia tutatengeneza maziwa ya unga
kwa ajili ya watoto, tutaanza kilimo cha umwagiliaji Busega pamoja na kuanzisha
kiwanda cha kutengeneza Tomato sauce; hapa kila wilaya ina jambo la kufanya,
hizi zote ni fursa ninyi askari na
viongozi changamkieni fursa zilizopo” alisisitiza.
Ameongeza kuwa kipindi cha miaka mitatu ijayo, Mkoa
wa Simiyu unatarajia kupunguza uagizaji wa bidhaa kutoka nje kwa asilimia 40% kwa kuwa vitaanzishwa viwanda vya kuchakata
mazao mbalimbali yanayopatikana hapa nchini katika kilimo, mifugo na uvuvi.
Wakati huo huo Mtaka amewataka askari wa jeshi la
polisi kutekeleza majukumu kwa kuzingatia maadili ya kazi yao ikiwa ni pamoja
na kupima nguvu ya kutumia kukabiliana na raia katika matukio mbalimbali na
kuepuka fedheha ya kuwa watoa taarifa kwa wahalifu.
Vile vile amewataka askari wote kuwa waangalifu
katika lugha wanayotumia wakati wakiwa wanatekeleza majukumu yao.
Wakati akimshukuru Mkuu wa Mkoa wa Mkoa kwa nasaha
mbalimbali alizotoa kwa Viongozi na Askari wa Jeshi la Polisi, Kamanda wa
Polisi wa Mkoa wa Simiyu, Boniventure Mshongi amewataka viongozi na askari
kufanya kazi zao kwa weledi huku wakizingatia maadili yao.
Katika kikao hicho viongozi na askari wa Jeshi la
Polisi wamewasilisha maoni, mapendekezo na maombi mbalimbali kwa Mkuu wa Mkoa
wa Simiyu ikiwa ni pamoja na kuomba Mamlaka za Serikali za Mitaa kupima na
kuwauzia viwanja kwa bei nafuu ili wajenge na kuendeleza Mkoa huo.
Maoni
Chapisha Maoni