KATIKA kuhakikisha uchochezi unaoweza kuvuruga amani ya nchi unadhibitiwa
wakati wa uchaguzi, Serikali imeiagiza Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA)
kuja na mwongozo wa kampuni za simu katika kudhibiti ujumbe mfupi kwa njia ya
simu.
Aidha, ameitaka sekta ya utangazaji nchini kutumia fursa ya Mkongo wa Taifa
katika utangazaji.
Hayo yalisemwa Dar es Salaam jana na Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia,
Profesa Makame Mbarawa alipokuwa akifungua maadhimisho ya Siku ya Teknolojia ya
Mawasiliano (ICT) Afrika.
Katika ujumbe wake kwa siku hiyo, alisema ujumbe mfupi wa kwenye simu
usipodhibitiwa unaweza kuleta madhara makubwa wakati wa uchaguzi.
“TCRA mje na mwongozo wa makampuni ya simu hasa kuhusu ujumbe, maana kama
utaachwa hivi hivi wakati wa uchaguzi itakuwa ni hatari, Kenya ilifanya hili na
walifanikiwa,” alisema.
Tayari TCRA imeshatengeneza miongozo ya namna ya kuripoti na kuandaa vipindi
wakati wa uchaguzi kwa upande wa sekta ya utangazaji na wamiliki wa mitandao ya
kijamii, yaani ‘blogers’.
Mbarawa alitumia nafasi hiyo kuvitaka vyombo vya utangazaji kutumia miongozo
waliyopewa katika kutangaza habari na zisizo na ushabiki na kutotumiwa vibaya na
baadhi ya watu.
Kuhusu Mkongo wa Taifa, Mbarawa aliitaka sekta ya utangazaji kutumia
ipasavyo fursa ya kuwapo kwa Mkongo wa Taifa katika matangazo yao.
Alisema Serikali imewekeza dola za Kimarekani milioni 200 (Sh bilioni 340)
katika teknolojia hiyo na kuwa sekta ya simu ndiyo pekee inayotumia na
kunufaika na teknolojia hiyo.
Mbarawa alisema ili kuhakikisha taasisi za utangazaji zinatumia Mkongo wa
Taifa, amemwagiza Katibu Mkuu wa Wizara yake kuunda timu ya wadau
itakayoangalia suala hilo.
Awali, Mkurugenzi wa TCRA, Profesa John Nkoma alisema teknolojia ya
mawasiliano nchini imekuwa na manufaa na kuchagiza maendeleo ya wananchi.
Nkoma alitolea mfano kuwa hadi sasa kuna laini za simu milioni 28 na laini
za intaneti milioni tisa na kuwa matumizi ya simu katika kufanya miamala ya
kibenki imeongezeka.
Naye Mratibu wa Ufundi wa Umoja wa Mawasiliano Afrika (ATU) “African
Telecommunications Union), Kezias Mwale aliipongeza Tanzania kwa kuwa miongoni
mwa nchi tatu za Afrika ambazo zimeshahamia kwenye dijitali na kuwa baadhi ya
nchi zimeahidi kufikia lengo hilo kabla ya muda uliowekwa kupita.
Tanzania inatarajiwa kuingia katika mwaka wa uchaguzi mwaka kesho, kwani
mbali ya kutarajiwa kupata Rais wa Awamu ya Tano atakayechukua nafasi ya Rais
Jakaya Kikwete anayemaliza muda wake, wananchi wanatarajiwa pia kupiga kura za
kuwapata wawakilishi wapya katika ngazi za majimbo na kata.
Aidha, kama sehemu ya mchakato wa uchaguzi mkuu ujao, mwishoni mwa wiki
ijayo Watanzania watafanya Uchaguzi wa Serikali za Mitaa utakaowaweka madarakani
viongozi wa vijiji, vitongoji na mitaa.
Maoni
Chapisha Maoni