WAKAZI wawili wilayani hapa, wamelazwa katika hospitali ya Wilaya ya
Kahama Mkoa wa Shinyanga baada ya kujeruhiwa katika mapigano kati yao
na askari Polisi, baada ya kumshika ugoni mmoja wa askari katika hoteli
moja maarufu mjini hapa.
Tukio hilo lilitokea juzi usiku baada ya mmoja wa vijana hao, kumkuta
askari akijivinjari na mkewe, ndipo alipomshirikisha ndugu yake na
kuibuka mapigano makali ya kurushiana makonde yaliyosababisha baadhi
yao kujeruhiana vibaya.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Shinyanga, Justus Kamugisha, alisema tukio
hilo limetokea baada ya askari, Sajenti Edward kufumaniwa akiwa na mke
wa mmoja wa vijana hao aliyejulikana kwa jina la Paschal Matonange
(26).
Kamugisha, alisema baada ya kufumaniwa akiwa na mwanamke huyo
chumbani, vijana hao walianza kumshushia kipigo huku wakimpiga picha
akiwa uchi, hali iliyosababisha vurugu kwenye hoteli hiyo iliyopo nje
kidogo na mji wa Kahama.
Kamanda huyo, alisema baada ya vurugu hizo wasamalia wema walijaa
eneo hilo na baadhi yao kupiga simu kituo cha polisi ambako askari
walifika kujaribu kutuliza vurugu hizo bila mafanikio.
Alisema katika kutuliza ghasia hizo, yalizuka mapigano makubwa kati
ya vijana hao na askari polisi, hali iliyosababisha kujeruhiwa kwa
baadhi ya askari na vijana hao ambao wamelazwa katika hospitali ya
Halmashauri ya Mji.
Aidha, waliolazwa ni pamoja Marco Matonange (27), na mdogo wake
Paschal Matonange ambaye ndie mme wa mwanamke huyo aliyefumaniwa akiwa
na askari.
Hata hivyo, Kamugisha alisema jeshi lake litamchukulia hatua za kinidhamu askari aliyefumaniwa na mke wa mtu, ambaye
pia
yumo kwenye kikosi maalumu cha kufanya uchunguzi wa makosa ya jinai, kwa kuwa kufanya hivyo ni utovu wa nidhamu.
“Kimsingi sisi kama polisi hatuhusiki na masuala ya ugoni na askari
kwenda pale kwenye tukio hawakwenda kwa ajili ya kufumania, bali
walikwenda kwa ajili ya kutuliza ghasia lakini ilikuwa ni kazi
kuwakamata hao vijana, mpaka sasa pamoja na wao kujeruhiwa pia baadhi ya
askari wamejeruhiwa,” alisema Kamugisha.
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Kahama, Benson Mpesya, alisema
suala hilo kwa kutumia nafasi yake ya uenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na
Usalama ya Wilaya, analifanyia kazi kwa mujibu wa taratibu na sheria
za nchi.
“Ni kweli tukio hilo ninalo, vyombo vyangu vya usalama vinalifanyia
kazi ikiwemo uchunguzi ili kujua hasa chanzo chake kilichosababisha
kuwepo kwa mapigano hayo,” alisema Mpesya ingawa mmoja wa majeruhi hao
alidai mkuu huyo ndie aliyewakoa wakati wakipata kipigo kituo cha
polisi baada ya kupiga simu kwa mkuu wa polisi Wilaya (OCD).
Akizungumzia tukio hilo katika Hospitali ya Mji wa Kahama, Mwenyekiti
wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Mkoa wa Shinyanga, Hamis Mgeja,
aliyefika kuwapa pole majeruhi, alisema jeshi la polisi linatakiwa
kufanya kazi kwa misingi ya sheria.
Mgeja, alimtaka Mkuu wa Jeshi la Polisi, (IGP), Ernest Mangu,
kuhakikisha anafanya uchambuzi wa askari wake wasiokuwa na nidhamu
ambao hutekeleza majukumu yao kwa vitisho, hali inayosababisha wananchi
kukosa imani nao.
Mganga mkuu wa Hospitali ya Mji wa Kahama, Deogratius Nyaga, alisema hali za majeruhi hao zinaendelea vizuri.
Maoni
Chapisha Maoni