IKULU YAKANUSHA KATIBU WA RAIS KUINGILA SAKATA LA ESCROW

VYOMBO vya habari nchini vimeaswa kuripoti matukio yaliyofanyiwa uchunguzi wa kina na yenye kufuata maadili na taaluma ya habari, badala ya kufanya kazi kwa kuongozwa na ushabiki vinapotekeleza majukumu yake.

Hayo yameelezwa katika taarifa ya Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais, Ikulu iliyotolewa jana kwa vyombo vya habari ikikanusha kuhusika kwa Katibu wa Rais Jakaya Kikwete, Prosper Mbena katika kumpa mwongozo Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Profesa Benno Ndulu ili auruhusu uchotwaji wa fedha katika akaunti ya Tegeta Escrow iliyopo katika BoT.

Taarifa hiyo inasema baadhi ya vyombo vya habari (siyo HabariLeo) vimemhusisha Mbena kuingilia mchakato wa uchotwaji wa zaidi ya Sh bilioni 306 katika akaunti hiyo iliyoibua hoja nzito nchini, kiasi cha Bunge kuingilia kati na kutaka baadhi ya mawaziri na watendaji serikalini wawajibike kwa kile kinachodaiwa kuchota fedha za umma, jambo ambalo bado halijathibitishwa rasmi. “Huu ni uongo na uzushi.

Ni jaribio jingine la kutia chumvi katika jambo ambalo limetawaliwa kwa kiasi kikubwa na mihemko ya aina yake.

Gavana Ndulu mwenyewe anathibitisha kuwa hajawahi kupokea barua yoyote kutoka kwa Katibu wa Rais kuhusu akaunti ya Tegeta Escrow.

Akaunti ya Escrow ilifunguliwa baada ya kutokea kwa mgogoro wa kimaslahi baina ya kampuni ya kufua umeme ya IPTL na Tanesco.

Maoni