MKAZI wa kijiji cha Chibwechangula –Behelo katika wilaya ya Mpwapwa mkoani
Dodoma, Ruth Matonya (26) amejifungua mtoto wa ajabu ambaye nusu ya sura yake
inafanana na binadamu na nusu ikifanana na chura.
Mtoto huyo alizaliwa Desemba 2, mwaka huu katika Kituo cha Afya cha
Mtakatifu Luka kinachomilikiwa na Kanisa la Anglikana, Dayosisi ya Mpwapwa.
Alifariki dunia muda mfupi baada ya kuzaliwa.
Kwa mujibu wa Mganga Mfawidhi wa kituo hicho, Dk Edwin Kihura mara baada ya
mama huyo kufika katika kituo hicho cha afya alikuwa na uchungu ambao haukuwa
na kikomo, lakini alishindwa kujifungua kwa njia ya kawaida licha ya njia ya
uzazi kufunguka.
Alisema kutokana na hali hiyo iliwalazimu kumfanyia upasuaji mama huyo kwa
lengo la kuokoa maisha yake na mtoto. Alisema wakati mama huyo akihudhuria
kliniki walipojaribu kupima miezi ya mwisho mama huyo, mkao wa mtoto ulikuwa
haupatikani pamoja na mapigo ya moyo lakini mtoto alikuwa anacheza tumboni
jambo ambalo lilikuwa likiwashangaza waganga na wauguzi kituoni hapo.
Dk Kihura alisema mara baada ya mama huyo kufanyiwa upasuaji waliweza kutoa
mtoto wa jinsi ya kike ambaye alikuwa na sura isiyoeleweka na kichwa kilikuwa
na sura ya binadamu na nusu ikiwa ni sura inayofanana na chura huku viungo
vingine vyote vya mwili vikiwa kamili.
Alisema zipo sababu kadha zinazoweza kusababisha tatizo kama hili ambapo
alisema kuwa ni baadhi ya akinamama kukosa baadhi ya madini mwilini na uumbaji
kutokamilika kutokana na sababu za kibaiolojia.
Alieleza kuwa hali ya mama huyo inaendelea vizuri na kwamba mtoto huyo
alikuwa ni mtoto wake wa tano.
Maoni
Chapisha Maoni