WANAFUNZI 46 wa chuo kipya cha kilimo na mifugo cha Nice Dream
kilichopo Mtaa wa Mapelele, Kata ya Ilemi jijini Mbeya wamejikuta wakiwa
katika wakati mgumu, baada ya kutelekezwa na uongozi wa chuo hicho,
kiasi cha kushindwa kupata chakula kwa siku tano mfululizo, hali
iliyosababisha baadhi yao kuzirai.
Hayo yameibuka baada ya uongozi wa chuo kudaiwa kuchukua ada za
wanafunzi hao, wengi wakiwa kutoka mikoa ya Kagera na Mara ambao
inaelezwa walitumiwa barua za kujiunga na chuo wakielezwa kuwa ni cha
Serikali, ilhali sivyo.
Aidha, mmiliki wake ametajwa kujaribu kukipa hadhi chuo kwa kutangaza
kuwa kimezinduliwa na Waziri Mkuu mstaafu, Frederick Sumaye ambaye naye
amekana kukitambua chuo hicho.
Hayo yamebainishwa na Diwani wa Kata ya Ilemi, Furaha Mwandalima
aliyesema alipokea malalamiko kutoka kwa wanachuo hao, naye kwenda
kujionea hali halisi katika chuo hicho alichosema hakuwahi kukisikia.
Baada ya kuiona hali ilivyokuwa, alilazimika kumtafuta Meya wa Jiji
la Mbeya, Athanas Kapunga aliyemshauri kutoa taarifa kwa Mkuu wa Wilaya
ya Mbeya, Dk Norman Sigalla ili kupata mustakabali wa suala hilo.
Mwandishi wa gazeti hili alifika chuoni hapo jana na kukuta baadhi ya
wanafunzi wakiwa wamedhoofu, huku mmoja wao akiripotiwa kuzirai kwa
kile kinachotajwa kuwa ni sababu ya njaa.
Hata hivyo, tatizo la njaa lilipata ufumbuzi wa muda baada ya wakazi
wa maeneo ya jirani na chuo kuchanga fedha na kuanza kuwapikia wanafunzi
hao.
Baadhi ya wananchi pia walionekana chuoni hapo wakiangua kilio kwa
kuwahurumia wanafunzi hao walioonekana dhahiri kuchanganyikiwa na tukio
la kutelekezwa kwao.
Mmoja wa wanafunzi hao, Joanes Renatus anayetoka mkoani Kagera,
alisema alipokea barua na fomu ya kutaarifiwa kujiunga na chuo hicho
baada ya matokeo ya kidato cha nne mwaka jana ikiambatanishwa na gharama
za michango yenye jumla ya Sh 860,000.
Alisema barua hiyo ilikuwa ikisisitiza mwanafunzi anatakiwa kuripoti
akiwa na karo ya muhula wa kwanza ambayo ni Sh 550,000 jambo ambalo
alilitekeleza kama ilivyokuwa kwa wanafunzi wenzake waliofika chuno hapo
Septemba mwaka huu.
Aliongeza kuwa, licha ya kutoka kwao akiwa na matumaini ya kupata
chuo kizuri, alipofika chuoni baada ya safari ya zaidi ya kilometa 1,200
kutoka Kagera hadi Mbeya, alishangazwa kuona mazingira yasiyoashiria
kuwa ni chuo alichopangiwa.
Na hata baada ya kutaka kujiridhisha, walibaini hakikuwa na usajili kutoka Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi (NACTE).
Wanafunzi wengine, Annaf Habibu kutoka Kagera na Mtani Ndelekule
kutoka Mara, wakifafanua zaidi walisema baada ya kuripoti chuoni hapo,
hawakukuta wanafunzi wengine na walipoulizia walijibiwa wamekwenda
katika mafunzo ya vitendo, kumbe sivyo, lakini kadri muda ulivyozidi
ikabainika kuwa wao walikuwa wanafunzi wa kwanza.
“Hatujui hatima yetu na tumetoka mbali kufuata elimu, lakini kumbe
sivyo…inauma zaidi kwa sababu wazazi wetu wamelazimika kuuza mifugo na
mashamba ili tusome, kumbe tunaishia katika mazingira haya…,” alisema
Ndelekule huku akilengwalengwa machozi.
Aliongeza kuwa, kwa kuwa imeshajionesha hakuna dalili za wao kusoma
chuoni hapo, ni vyema kama Serikali ikawasaidia kupata vyuo vingine ili
watimize ndoto zao na pia kuwafuta `machozi’ wazazi wao.
Kutokana na adha hiyo, Diwani Mwandalimi alisema mwafaka uliofikiwa
ni kutolewa kwa agizo la kuorodheshwa kwa majina ya wanafunzi na mahali
wanakotoka ili kuwarudisha makwao na chuo kifungwe kutokana na
kutosajiliwa rasmi na kwamba kilikuwa kinaendeshwa kijanja.
Balozi wa Mtaa wa Mapelele, Geophrey Mwalupindi na mkazi mwenzake
Fanuel Kisanga walipoulizwa juu ya chuo hicho, walionesha kushangazwa na
taarifa hizo, huku wakisema awali kilikuwa ni kituo cha kufundishia
masomo ya ziada (twisheni) na shule ya chekechea.
Kati ya wanafunzi waliotapeliwa, 41 wanatokea Mkoa wa Kagera, wawili
mkoani Mara, wawili wilayani Kyela mkoani Mbeya na mmoja akitokea Dar es
Salaam.
Juhudi za kuupata uongozi wa chuo hicho haukufanikiwa kupitia namba
za simu za mkononi walizoandika kwenye bango la chuo ambazo ni
0765659079 na 0684423849, kwani hazikupatikana hewani.
Uchunguzi pia umebaini malipo ya karo chuoni hapo yalikuwa
yakipokelewa kwa ujanjaujanja na mtu aliyefahamika kama Samwel Daudi
ambaye ni mmiliki wa chuo hicho na njia anazotumia kukusanyia ada kutoka
kwa wanafunzi ambao hupeleka kwa Katibu Muhtasi wake na kutoa
stakabadhi isiyokuwa na namba za usajili wa chuo wala namba za TRA.
Njia nyingine ambayo wanafunzi waliambiwa walipie ada zao ni kupitia
njia ya M-Pesa ambapo mzazi alilazimika kutuma kwa wakala mwenye namba
98369 tofauti na kupokelewa kwa njia ya benki au simu ya uongozi.
Kama vile haitoshi, mmiliki wa chuo hicho alitumia mbinu zaidi ili
kuwaaminisha wanafunzi na wazazi kuwa chuo hicho kimesajiliwa baada ya
kuchora kibao kikionesha chuo hicho kilifunguliwa rasmi na Waziri Mkuu
mstaafu, Sumaye.
Hata hivyo, gazeti hili lilipomtafuta Sumaye kuzungumzia
anavyokifahamu chuo hicho kinachojinadi kimezinduliwa naye Oktoba 24,
mwaka huu, alikana kuhusika nacho.
“Sijafika chuoni hapo na wala sikijui. Huyo aliyefanya hivyo ni
tapeli, anapaswa kuchukuliwa hatua za kisheria,” alisema akionekana
kuguswa na tukio hilo.
Aliongeza kuwa, alialikwa kwa shughuli ya kanisa mjini Mbeya na akiwa
huko alifuatwa na mmiliki wa chuo akimwomba kufungua chuo chake, lakini
akakataa kwa kuwa alishapata taarifa za awali, hivyo kumshauri mmiliki
huyo kukamilisha taratibu zinazotakiwa ndipo amwite kwa uzinduzi rasmi.
“Si zaidi ya hapo, ametumia vibaya jina langu na hakika hicho ni kitu kibaya kweli kweli…,” alisema Sumaye.
Maoni
Chapisha Maoni