KONGAMANO la wakuu wa mikoa kuhusu ajira linatarajiwa kufanyika kwa
siku mbili mkoani hapa kuanzia leo likishirikisha watu zaidi ya 200,
imefahamika.
Madhumuni ya kongamano hilo ni kuwakutanisha wakuu wa mikoa na wadau
mbalimbali kujadili kuhusu changamoto ya ukosefu wa ajira kwa vijana na
kupendekeza mikakati ya kukuza fursa za ajira nchini.
Waziri wa Kazi na Ajira, Gaudentia Kabaka aliwaambia waandishi wa
habari jana mjini hapa kuwa kongamano hilo limeandaliwa na wizara yake
kwa kushirikiana na Shirika la Kazi Duniani (ILO) na Taasisi ya Utafiti
wa Masuala ya Uchumi na Kuondoa Umasikini (REPOA).
Kabaka alisema wajumbe zaidi ya 200 wakiwamo wakuu wa mikoa yote ya
Tanzania Bara, makatibu tawala wa mikoa, wadau wa maendeleo, wakuu wa
taasisi za umma na zisizo za kiserikali, sekta binafsi na vikundi vya
vijana, watashiriki kongamano hilo.
“Kongamano hili la kitaifa litafanyika tarehe 19 na 20 Novemba,
katika Ukumbi wa Mtakatifu Gaspar na litafunguliwa na Mheshimiwa Waziri
Mkuu Mizengo Kayanza Pinda,” alisema Kabaka.
Alisema wakuu wa mikoa wataandaa na kusaini Azimio la namna
watakavyosimamia utekelezaji wa mikakati ya kukuza uchumi kwa vijana
nchini pamoja na mwongozo wa utekelezaji.
Alisema kaulimbiu ya Kongamano hilo ni “Ni wakati wa kuwawezesha
vijana,” ikiwa na maana sasa si wakati tena wa kupanga kufanya nini,
bali kuwawezesha vijana kwa kutumia fursa zilizopo katika maeneo yao.
“
Katika kongamano hilo, mada mbalimbali zitawasilishwa na kujadiliwa na
hatimaye kuandaa mikakati ya kukuza fursa za ajira ambayo itakuwa ni
sehemu ya Azimio la Wakuu wa Mikoa,” alisema Kabaka.
Maoni
Chapisha Maoni