KAMPUNI 12 zimejitokeza kuwania zabuni ya kujenga barabara mbadala
kati ya Dar es Salaam hadi Chalinze kwa kiwango cha Expressway ambayo
itakuwa ya kulipia.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Uhusiano na Uratibu, Steven Wasira
aliyasema hayo juzi bungeni wakati akichangia Muswada wa Marekebisho ya
Sheria ya Ubia baina ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi (PPP).
Bila ya kutaja majina ya kampuni hizo, Wasira alisema kampuni hizo 12
zimejitokeza kuwania zabuni ya ujenzi huo ambao utajengwa kwa utaratibu
huo wa PPP.
Jana asubuhi, wakati wa kipindi cha maswali na majibu bungeni, Naibu
Waziri wa Ujenzi, Gerson Lwenge, alibainisha kuwa mojawapo ya hatua
zinazochukuliwa na Serikali kuimarisha barabara ya Morogoro, ni ujenzi
wa Expressway kutoka Dar es Salaam hadi Chalinze.
Alipowasilisha bungeni makadirio ya wizara kwa mwaka wa fedha
2014/15, Mei 23, mwaka huu, Waziri wa Ujenzi, Dk John Magufuli alisema
barabara hiyo mbadala itakuwa ya kulipia, na itajengwa kwa njia sita
(lanes).
Dk Magufuli alisema barabara ya sasa itaendelea kutoa huduma kwa wale
ambao hawako tayari kulipia. Barabara hiyo ina urefu wa kilometa 100.
Katika hatua nyingine, Serikali imesema itaajiri watumishi wa ardhi
220 ambao kipaumbele kitapewa maeneo ambayo hayana watumishi wengi wa
sekta hiyo.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma,
Celina Kombani, alisema hayo jana bungeni akijibu swali la nyongeza la
Mbunge wa Ileje, Aliko Kiboba (CCM).
Kombani alisema watumishi hao watapelekwa katika maeneo yenye
upungufu wa watumishi hao ikiwamo Wilaya ya Ileje, kama alivyoomba
Mbunge Kibona.
Maoni
Chapisha Maoni