SHULE YA FILBERT BAYI YATEKETEA KWA MOTO.

SHULE ya msingi ya bingwa wa zamani wa dunia wa mbio za mita 1500, Filbert Bayi imeteketea kwa moto usiku wa kuamkia jana, imeelezwa.

Bayi akizungumza jana kwa njia ya simu kutoka Mkuza, Kibaha iliko shule niyo alisema kuwa, shule hiyo imeteketea kabisa kwa moto na hakuna kilichookolewa, lakini hakuna mwanafunzi aliyejeruhiwa.

Alisema kuwa gharama ya shule hiyo yenye wanafunzi 280 huku 69 wakiwa ni wa bweni, ni zaidi ya Sh milioni 700 na moto huo huenda ungedhibitiwa kama Zimamoto Pwani wangefika mapema.

Bayi, ambaye pia ndiye Katibu Mkuu wa Kamati ya Olimpiki Tanzania (TOC), alisema kuwa watoto hao wa bweni walitoka tu na nguo zao za kulalia huku vitu vingine vyote vikiteketea kabisa.

Alisema pamoja na kwenda mwenyewe katika ofisi za Zimamoto Kibaha kuomba msaada wa gari la kuzima moto, aliambiwa kuwa gari lilikuwa bovu, hivyo lilishindwa kwenda kuzima moto na hadi magari ya zimamoto yalipotoka Dar es Salaam kwenda kuzima, moto huo uliokwishateketeza kila kitu.

Alisema wakati anakwenda katika ofisi za Zimamoto Kibaha, moto ulikuwa haujapamba na vitu vingi kama madarasa, mabweni, bwalo la chakula na darasa la kompyuta visingeteketea kabisa kama gari hilo lingefika mapema.

Bayi alitoa lawama kwa Idara ya Zimamoto Kibaha kwa kutokuwa tayari kwa majanga, ambapo aliwataka kuboresha vifaa vyao ili waweze kukabiliana na moto kwa wakati pale unapotokea.

Alisema kuwa kwa sasa wanafunzi wa shule hiyo wanakaa na kusomea katika baadhi ya madarasa ya shule ya sekondari ya Filbert Bayi ambayo iko jirani na ilipokuwa hiyo iliyoungua.

Kamanda wa Polisi mkoa wa Pwani, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi, Ulrich Matei alikiri kutokea kwa ajali hiyo ya moto na kusisitiza kuwa Polisi waliwahi kufika na kuweka ulinzi katika shule hiyo ili vibaka wasiibe vitu, lakini wenzao wa Zimamoto walishindwa kutokea sababu gari lao lilikuwa bovu.

Alisema Zimamoto kutoka Dar es Salaam ndio waliofika kuuzima moto huo ulioanza majira ya saa 8 za usiku, ambao tayari ulishateketeza kila kitu, na alitaka suala la Zimamoto aulizwe kamanda wao.

Alisema wao kama Polisi walifanya kazi yao ya kulinda usalama eneo la tukio, lakini suala la Zimamoto sababu za kuwa na gari moja na bovu waulizwe wenyewe kwani ni idara kamili inayojitegemea.

“Sisi kama Polisi tulifanya kazi yetu ya kulinda usalama, lakini kuhusu Zimamoto kuwa na gari moja na bovu hilo waulizwe wenyewe kwa kuwa wao ni idara kamili inayojitegemea, “alisema Kamanda Matei.

Alisema moto huo ulianzia katika bweni la wasichana lililokuwa na wanafunzi 39 na kuendelea katika maeneo mbalimbali ya shule ikiwemo bwalo la kulia chakula, madarasa na maeneo mengine.

Juhudi za kumpata msemaji wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji nchini, Inspekta Puyo Nzalayaimisi kuzungumzia tukio hilo hazikuzaa matunda, licha ya kutafutwa mara kadhaa kwa simu yake ya mkononi.

Maoni