MTUHUMIWA wa vitendo vya ujambazi kutoka Kijiji cha Masangura, Wilaya ya
Kurya West nchi jirani ya Kenya, Chacha Marwa Gibai maarufu kama Mapengo
anashikiliwa na polisi katika Kanda Maalumu ya Tarime/Rorya akituhumiwa kuua
mtu kwa kumchoma kisu na kujeruhi mwingine kwa kisu katika vurugu aliyoianzisha
baa mjini hapa.
Kukamatwa kwa Mapengo kumethibitishwa na Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya
Tarime/Rorya, Lazaro Mambosasa aliyesema mtuhumiwa huyo anadaiwa kumchoma kisu
kifuani na tumboni mkazi wa mjini Tarime, Isack Mwita Matutu (20) na
kumsababishia kifo kabla ya kumshambulia mfanyabiashara Deus Tenten pia wa hapa
aliyejeruhiwa shingoni.
Kamanda Mambosasa, akielezea mkasa huo, alisema: “Tukio hilo la mauaji ya
kijana Isack Mwita Matutu yalitokea saa 4 usiku wa kuamkia Jumatano (jana)
katika Baa ya Criss Pub ambapo kulitokea ugomvi kati ya mtuhumiwa na marehemu
alikuwa akinywa na wenzake katika baa hiyo ambapo mtuhumiwa alichomoa kisu na
kumchoma Isack kifuani na tumboni na kufariki muda mfupi kabla hajafikishwa
katika Hospitali ya Wilaya kwa matibabu.
“Lakini pia akamjeruhi mfanyabiashara Deus Tenten shingoni ambapo majeruhi
alikimbizwa hospitali haraka na kutibiwa na hali yake haijaimarika. Tunamshikilia
Chacha Mapengo kwa mahojiano zaidi. Naye anatibiwa kwa sababu alishambuliwa na
wananchi kabla ya kuokolewa na askari wetu waliowahi eneo la tukio.”
Alisema mtuhumiwa huyo anahusishwa kutishia watu maisha, na kwamba tayari
ana kesi katika Mahakama ya Wilaya Tarime ya kumtishia maisha Meneja wa Mamlaka
ya Mapato (TRA), Mkoa wa Mara Ben Usaje.
Pia ana kesi ya kumchoma kisu tumboni mkazi wa Sirari, wilayani hapa aitwaye
Soko Waisaki na kumsababishia ulemavu.
Maoni
Chapisha Maoni