MJADALA WA ESCROW WAWA MOTO BUNGENI.

RIPOTI ya Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) kuhusu kuchotwa kunakodaiwa isivyo halali kwa fedha katika Akaunti ya Escrow, sasa haitajadiliwa bungeni.

Naibu Spika wa Bunge, Job Ndugai aliyasema hayo bungeni mjini hapa jana alipokuwa akijibu Mwongozo wa wabunge kuhusu kujadiliwa kwa ripoti za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) na Takukuru kuhusu sakata hilo.

Mwongozo wa awali kwa suala hilo ulitolewa na Mbunge wa Nyamagana, Ezekiah Wenje (Chadema) aliyehoji kutoonekana kwa ripoti ya Takukuru katika ratiba ya vikao vya Bunge na badala yake kuonekana ripoti ya CAG.

Kwa mujibu wa ratiba mpya ya Bunge iliyotolewa juzi, inaonesha kuwa ripoti ya CAG kuhusu sakata hilo la fedha katika akaunti ya Escrow, itawasilishwa katika Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) ambayo Mwenyekiti wake ni Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe (Chadema), Novemba 26, mwaka huu.

Akijibu Mwongozo huo wa Wenje na baadaye wa Mbunge wa Arumeru Mashariki, Joshua Nassari (Chadema), kuhusu kwa nini ripoti ya Takukuru haitaletwa kujadiliwa bungeni, Ndugai alisema kwa mujibu wa sheria, Takukuru hawapaswi kuwasilisha ripoti yao bungeni.

“Waheshimiwa wabunge Takukuru wao wakimaliza kazi yao, na wakibaini kuna makosa ya jinai, inachukua hatua moja kwa moja kwa kuwasiliana na DPP (Mkurugenzi wa Mashitaka) na kuwafikisha wahusika mahakamani,” alisema Ndugai.

Aidha, Naibu Spika huyo akijibu hoja za wabunge hao kwamba kuna usiri na kampeni zinafanywa katika kushughulikia suala hilo tangu lilipotua bungeni, alisema hakuna usiri wowote unaofanywa kwani hatua zinazochukuliwa ni zile zilizofikiwa na Kamati ya Uongozi ya Bunge ilipojadili sakata hilo.

Alisema kwa mujibu wa Kanuni za Bunge, ripoti hiyo ni lazima ipite kwenye Kamati ya PAC kabla ya kujadiliwa bungeni, na kwamba kupangwa kwa kikao hicho mwishoni mwa shughuli za Mkutano wa 16 na 17 wa Bunge unaoendelea ni utaratibu wa kawaida.

“Waheshimiwa wabunge kitendo cha suala hili la Escrow kupangwa tarehe hiyo ni suala la kawaida kwa shughuli za kibunge. Kama mnavyofahamu kwa kawaida Bunge huanza kwa kujadili shughuli za serikali na zile za kamati huwekwa mwishoni mwa vikao vyetu,” alisema Ndugai.

Hata hivyo, hatua ya ripoti hiyo ya Takukuru kutangazwa kutowasilishwa bungeni kulimfanya Zitto kusimama na kueleza kuwa ili Kamati yake iweze kufanya kazi ipasavyo katika kuipitia ripoti ya CAG ni lazima ripoti hiyo iambatane na ripoti ya Takukuru.

Hatua hiyo ilimfanya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Kazi Maalumu anayekaimu nafasi ya Waziri Mkuu bungeni, Profesa Mark Mwandosya kusimama na kulieleza Bunge kuwa Kamati ya PAC ina mamlaka ya kuwaita Takukuru wakati itakapokuwa inajadili ripoti ya CAG.

Alisema kimsingi si kwamba serikali inazuia kuwasilishwa kwa ripoti ya Takukuru, bali suala hilo linatokana na matakwa ya kisheria, lakini akasema Takukuru wanaweza kuwasilisha kwa Kamati ya Bunge aina nyingine ya ripoti itakayosaidia kamati kufanya kazi yake kikamilifu.

Maoni