SERIKALI imesema maandalizi kwa ajili ya uchaguzi wa Serikali za
Mitaa unaotarajiwa kufanyika kote nchini Desemba 14, mwaka huu,
yamekamilika ikiwa ni pamoja na kusambazwa kwa masanduku ya kupigia kura
na kwamba unatarajiwa kugharimu Sh bilioni 20.
Aidha, katika mchakato huo, vyama vya siasa vitaruhusiwa kuweka mawakala wao na gharama za mawakala zitalipwa na vyama husika.
Katika mkutano wake na waandishi wa habari jana, Mkurugenzi wa Idara
ya Serikali za Mitaa katika Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na
Serikali za Mitaa, Khalist Luanda alisema maandalizi ya uchaguzi huo
yamekamilika.
Alisema gharama za uchaguzi huo, zinahusisha utengenezaji wa
masanduku, kusafirisha masanduku hadi kwenye vituo vya kupigia kura,
kusambaza vifaa na fomu mbalimbali pamoja na gharama za usimamizi wa
uchaguzi huo hadi utakapokamilika.
Alisema Waziri Mkuu ndiye aliyepewa madaraka ya kutunga kanuni za
kusimamia uchaguzi huo na tayari kanuni hizo zimewekwa kwenye mtandao wa
wizara.
“Tayari masanduku ya kupiga kura yamesambazwa kwenye halmashauri zote
nchini pamoja na fomu mbalimbali na vifaa vyote kwa ajili ya uchaguzi
viko tayari,” alisema.
Alisema uandikishaji wa wapiga kura, utafanyika kwa kutumia Rejesta
ya Wakazi, badala ya kutumia Daftari la Kudumu la Wapigakura ambalo
linatumika katika uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani.
Alisema sababu kubwa ya kutotumia daftari la kudumu la wapiga kura ni
kwa kuwa daftari hilo limeandaliwa kwa kuzingatia ukazi wa watu, mwisho
katika ngazi ya kata.
Alisema uandikishaji utafanyika kwa kuwaorodhesha wakazi wenye sifa
za kupiga kura kwenye rejista, zitakazokuwa katika vituo vya
kuandikishia wapiga kura na vituo hivyo vitaandaliwa na wasimamizi
wasaidizi wa uchaguzi.
Pia, alisema uandikishaji wa orodha ya wapigakura, utafanyika kwenye
majengo ya umma na pale ambapo hakuna jengo la umma, uandikishaji
utafanyika kwenye sehemu ambayo msimamizi msaidizi wa uchaguzi, atakuwa
amekubaliana na viongozi wa vyama vya siasa.
Alisema wanaoruhusiwa kuchukua fomu kwa ajili ya kugombea ni wale
walio na umri kuanzia miaka 21; na wenye umri wa miaka 18 hawataruhusiwa
kugombea, wao watabaki kuwa na sifa ya kuwa wapiga kura.
Mkurugenzi huyo alisema wasimamizi wa uchaguzi, wataandaa fomu za
kugombea na kila fomu itakuwa na nembo ya halmashauri na nembo ya chama
cha siasa chenye wagombea.
Alisema kila msimamizi wa uchaguzi, atahakikisha zinakuwepo fomu za
kutosha za wagombea kwa uchaguzi wa viongozi wa vijiji, mitaa na
vitongoji kulingana na nafasi zinazogombewa na fomu hizo zitatolewa bila
masharti au malipo yoyote.
Alisema kutatolewa nakala mbili kwa kila ombi la mwombaji, nakala
moja ya fomu baada ya kujazwa na mgombea na baada ya uteuzi itabandikwa
nje kwenye ubao wa matangazo ili mgombea yeyote mwenye pingamizi
ajitokeze; na nakala ya pili itabaki ofisini kwa msimamizi msaidizi wa
uchaguzi kwa ajili ya kutunza kumbukumbu.
Pia, msimamizi wa uchaguzi kwa maana ya mkurugenzi wa mamlaka ya
Serikali za Mitaa, atateua Ofisa wa umma ambaye ataandikisha na kuandaa
orodha ya wapigakura katika kitongoji kwa ajili ya uchaguzi wa
Mwenyekiti wa Kijiji, wajumbe wa halmashauri ya kijiji na mwenyekiti wa
kitongoji siku 21 kabla ya siku ya uchaguzi, ambayo ni Novemba 23, mwaka
huu.
Alisema uandikishaji wa wapiga kura utafanyika kwa siku saba kuanzia Novemba 23 hadi Novemba 29, mwaka huu.
Alisema msimamizi wa uchaguzi atabandika orodha ya wapigakura mahali
pa matangazo ya uchaguzi Novemba 30, mwaka huu na kutunza kumbukumbu
yake.
Pia, orodha ya mwisho ya wapiga kura itabandikwa siku tatu kabla ya
siku ya uchaguzi, ikiwa ni kuanzia Desemba 11 hadi Desemba 13, mwaka
huu.
Maoni
Chapisha Maoni