WANASIASA ACHENI KUINGILIA NEC.

WASOMI na wadau mbalimbali wamepongeza juhudi za Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) za kuboresha Daftari la Wapigakura na wamewataka wanasiasa waache kuingilia tume hiyo.

Wametaka tume hiyo iachwe ifanye kazi hiyo bila kuingiliwa na wanaolalamikia kutoshirikishwa, waelewe kuwa kazi hiyo ni ya NEC na inafanyika kitaalamu.

Wakizungumza na HabariLeo jana, walitaka kila mmoja kubaini kuwa suala hilo ni muhimu kwa nchi ya kidemokrasia, hivyo kuepuka kuwapotosha wananchi kwa kuingilia utendaji kazi wa Tume hiyo.

Mchambuzi wa masuala ya siasa na Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dk Benson Bana alisema ni lazima kutambua kuwa serikali inajua wajibu wake, hivyo suala la NEC kupewa Sh bilioni 15, badala ya Sh bilioni 293 zinazotakiwa, zisiwape tabu wananchi na wanasiasa.

Alisema hakuna haja ya kuogopa, kwani Serikali inatoa fedha hizo Hazina na inatambua umuhimu wa uboreshaji wa Daftari, kwani wanaochambua gharama za matumizi ya serikali ni Hazina na serikali ina bajeti ya kutosha.

Dk Bana alisisitiza kuwa kwa sasa ni wakati muafaka kuandikisha upya wapigakura, kwani ni haki ya kila Mtanzania. Alisema jambo la msingi kwa wadau wa siasa na asasi za kiraia ni kwenda katika mikoa yote hadi vijijini, kuhamasisha watu wajiandikishe.

Alisema suala hilo ni lazima kufanyika haraka, kwani ni jambo zuri; na sasa linakuwa la kitaalamu zaidi, kwa kutumia mfumo wa elektroniki. Alitaka watu waache maneno ya kukwamisha suala hilo, bali waiachie Tume na wataalamu.

Akizungumzia suala la baadhi ya wanasiasa kulalamika kutoshirikishwa, alisema anawashangaa wanataka kushirikishwa katika masuala yapi, kwani kila mmoja ana majukumu yake.

Alisisitiza kuwa wanasiasa hawana utaalamu, wala siyo kazi yao kununua vifaa vya uchaguzi. Mhadhiri wa UDSM na mmoja wa waanzilishi wa chama kipya cha siasa cha ACT, Profesa Kitila Mkumbo alisema NEC imeonesha dhahiri kuwa wao kazi wanaweza kuifanya kwa muda huo.

Alisema tatizo kubwa ni bajeti, hivyo aliomba serikali kutafuta kila njia kuhakikisha wanapata fedha za kuboresha Daftari la Wapigakura. Alisema Daftari la Wapigakura ni jambo la msingi, kwani wananchi wengi hawapo na wadau wa siasa wamekuwa wakilalamikia wapigakura wachache hivyo ni vyema kuunga mkono ili lifanikiwe.

“Demokrasia ni muhimu katika nchi na ina gharama, hivyo Serikali inatakiwa kutafuta fedha ili kufanikisha suala hili. Inakadiriwa kuwa watu zaidi ya milioni nne hadi tano hawapo kwenye daftari hili la sasa, hivyo uboreshaji utaondoa malalamiko ya wadau,” alisema.

Akizungumzia ushirikishwaji, alitaka wadau kuacha kuzua sababu, kwani hata kama wakishirikishwa kwa kiasi gani, NEC ndiyo wenye jukumu la kufanya kazi hiyo, hivyo ni vyema kushirikiana kuhakikisha wote wenye sifa wanajiandikisha kwenye daftari hilo.

Mwenyekiti wa chama cha DP, Christopher Mtikila alidai daftari hilo halitakuwa sahihi, kwani linatengenezwa na watu wa upande mmoja wenye madhumuni yao.

Alitaka wadau wote kukaa pamoja na kujadiliana jinsi ya kuliboresha. Alidai suala la uboreshaji, limegubikwa na utata kuanzia masuala ya zabuni na kwamba wahusika hawajachukuliwa hatua zozote, jambo ambalo linatoa shaka kwa wadau wengine.

Juzi NEC ilitangaza rasmi kuanza kuboresha Daftari la Wapigakura kuanzia mwezi ujao na kwamba itakamilisha kazi hiyo Aprili 18 mwakani.

Maoni