WAFANYAKAZI 200 RELI KUKOSA MAFAO,

WAFANYAKAZI zaidi ya 200 wa lililokuwa Shirika la Reli Tanzania (TRC), hawatalipwa mafao yao baada ya kujitoa kwenye kesi ya kudai fedha hizo.

Hayo yamebainika siku moja baada ya Tume ya Usuluhishi na Migogoro ya Kazi (CMA)kulitaka Shirika Hodhi la Reli (RAHCO) la mali zilizokuwa chini ya TRC, kuwalipa mafao wafanyakazi 1,500 waliokuwa wameajiriwa na TRC.

Imeelezwa kuwa wafanyakazi hao zaidi ya 200, walikuwa na haki ya kulipwa mafao yao ya kustaafu, lakini walijitoa katika kesi hiyo, kutokana na kukimbia gharama za kesi na kukata tamaa.

Katibu Mkuu wa Chama cha Wafanyakazi wa Reli Tanzania (TRAWU), Erasto Kihwele alisema wafanyakazi hao zaidi ya 200 walipojitoa katika kesi hiyo, walibaki wenzao 1,500 ambao ndio walioshinda kesi.

Hata hivyo, Kihwele alisema wafanyakazi hao zaidi ya 200, wana nafasi ya kufungua kesi nyingine ya madai, kwani vielelezo vyote vipo. Kihwele alisema CMA imeamuru RAHCO iwalipe wafanyakazi hao 1,500 mafao yao ya Sh bilioni 16.2 ndani ya siku 90.

“Sisi tunataka walipe fedha husika ndani ya siku 90 ili kutekeleza uamuzi huo wa Mahakama,” alisema.

Pia, alibainisha kuwa ikiwa maamuzi hayo ya CMA, hayatatekelezwa ndani ya siku 90, chama hicho kitaenda CMA kukazia hukumu kutekeleza maamuzi hayo ya Tume na kama wataendelea kukaidi, watapeleka suala hilo mahakama za juu ili haki itendeke.

Alisema wafanyakazi hao, wanatakiwa kulipwa na RAHCO ambao wamehodhi mali zilizokuwa chini ya TRC, kabla ya mkataba baina yao na shirika hilo kukoma. Baada ya kukoma, ilianzishwa Kampuni ya Reli Tanzania (TRL) ambayo inaendelea kuendesha Reli ya Kati.

Mmoja wa maofisa wa TRL ambaye si msemaji wa suala hilo, alisema mzungumzaji wa suala hilo ni Ofisa Mtendaji Mkuu wa RAHCO, Benhadard Tito ambaye kwa sasa yupo safari nje ya nchi, kutokana na kuwa suala hilo ni la kisera.

“Mimi siwezi kuzungumza kwa sababu si msemaji na pia mi mwenyewe ni kati ya wafanyakazi hao tunaopaswa kulipwa mafao hayo na tunasubiri kulipwa,” alisema.

Gazeti hili lilipomtafuta Tito kulizungumzia suala hilo, simu yake kwa mara ya kwanza ilikuwa ikiita bila majibu ;na baadaye ilipopigwa tena, ikakatwa na haikupatikana tena. Uamuzi wa CMA umetolewa mjini Tabora na Mwenyekiti wa CMA, Adolf Anosisye.

Katika uamuzi huo, Mwenyekiti huyo wa CMA ameipa siku 90 RAHCO kutekeleza uamuzi huo wa kushughulikia mafao hayo ya wafanyakazi hao wa iliyokuwa TRC.

Alisema RAHCO inawajibika kisheria kushughulikia malipo ya wafanyakazi hao na kuwalipa mafao yao ya kustaafu. Madai ya msingi, yaliwasilishwa kwenye tume hiyo na Japhet Mkoba kwa niaba ya wafanyakazi 1,500 waliokuwa waajiriwa wa TRC.

Mkoba na wenzake katika madai yao, walidai kulipwa jumla ya Sh bilioni 16.2 na TRC baada ya mkataba wa utumishi baina yao kukoma mwaka 2007, hivyo madai yao ya kulipwa mafao ya mwisho ya utumishi wao kuachwa mikononi mwa RAHCO.

Waliamua kufungua mashauri katika Tume hiyo baada ya kupigwa danadana na RAHCO na TRL, ambao kila mmoja alikuwa akisukuma jukumu hilo kwa mwingine.

Walalamikaji katika shauri hilo walikuwa wakiwakilishwa na Mawakili Iddi Ndabhona na Alphonce Sabukoto wa Kampuni ya Uwakili ya Kigoma Lake Tanganyika ya mjini Kigoma. 

Walalamikiwa, RAHCO, waliwakilishwa na Wakili M.K.Mtaki.

Maoni