TUME ya Usuluhishi na Migogoro ya Kazi (CMA) imelitaka Shirika Hodhi
la Reli (RAHCO) la mali zilizokuwa chini ya Shirika la Reli Tanzania
(TRC), kuwalipa mafao yao wafanyakazi 1,500 waliokuwa wameajiriwa na
TRC, kabla ya mkataba baina yao na shirika hilo kukoma.
Uamuzi wa tume hiyo umetolewa mjini Tabora na Mwenyekiti wa CMA,
Adolf Anosisye. Katika uamuzi huo, Mwenyekiti huyo wa CMA ameipa siku 90
RAHCO kutekeleza uamuzi huo wa kushughulikia mafao hayo ya wafanyakazi
hao wa iliyokuwa TRC.
Anosisye alisema amefikia uamuzi huo, baada ya kupitia vielelezo
mbalimbali vilivyowasilishwa kwenye tume hiyo na pande mbili
zinazosigana kwenye mgogoro huo.
Alisema RAHCO inawajibika kisheria kushughulikia malipo ya
wafanyakazi hao na kuwalipa mafao yao ya kustaafu. Madai ya msingi,
yaliwasilishwa kwenye tume hiyo na Japhet Mkoba kwa niaba ya wafanyakazi
1,500 waliokuwa waajiriwa wa TRC.
Katika madai hayo, wafanyakazi hao wanaitaka Tume kutoa maamuzi ya
kisheria ya kulipwa mafao yao na RAHCO, ambayo imepewa mamlaka ya
kusimamia ufilisi wa mali na madeni ya TRC.
Mkoba na wenzake, katika madai yao hayo, wanadai walipwe jumla ya Sh
bilioni 16.2 na lililokuwa Shirika la Reli Tanzania (TRC) baada ya
mkataba wa utumishi baina yao na shirika hilo kukoma mwaka 2007, hivyo
madai yao ya kulipwa mafao ya mwisho ya utumishi wao kuachwa mikononi
mwa RAHCO.
Akizungumza na gazeti hili, Mkoba alisema kuwa waliamua kufungua
mashauri katika Tume hiyo ya Usuluhishi baada ya kupigwa danadana na
RAHCO na Kampuni ya Reli Tanzania (TRL), ambao kila moja ilikuwa
ikisukuma jukumu hilo kwa mwingine.
Maoni
Chapisha Maoni