TUME ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) imetangaza rasmi kuanza kuboresha Daftari la
Wapigakura kuanzia mwezi ujao na kwamba itakamilisha kazi hiyo Aprili 18
mwakani.
Kwa tangazo hilo la NEC, ni wazi kuwa upigaji wa kura ya maoni juu ya Katiba
Inayopendekezwa, utafanyika siku chache tu baada ya kukamilika kazi ya
uboreshaji wa daftari hilo; na baadaye litatumika kwa uchaguzi mkuu ujao.
Hata hivyo, tume hiyo imeonesha wasiwasi wa kukamilisha kazi hiyo kwa
wakati, kutokana na serikali kusuasua kutoa fedha za kufanyia uboreshaji huo,
kwani hadi sasa NEC imepatiwa Sh bilioni 15 tu kati ya Sh bilioni 293
zinazohitajika.
Ucheleweshaji wa kutoa fedha hizo, umekuwa ukilalamikiwa na tume hiyo kuwa
unachelewesha uboreshaji huo, ambao awali ulikuwa uanze Septemba, lakini
umekuwa ukisogezwa mbele kusubiri fedha kutoka serikalini.
Naibu Katibu Mkuu wa Uandikishaji Wapigakura wa NEC, Sisti Cariah alisema
hata hivyo wana matumaini makubwa ya kupata fedha zote kwa wakati na kwamba
daftari hilo litakamilika ifikapo Aprili 18 na wanatarajia kuandikisha
wapigakura milioni 23.9.
“Uandikishaji huu unafanyika kwa haraka ili itakapofika wakati wa kupiga kura
za maoni (ya Katiba Inayopendekezwa) daftari liwe limekamilika jambo ambalo
tunaamini litakamilika kwa wakati,” alisema.
Juni mwaka huu, NEC ilitangaza kutoa vitambulisho vipya vya kupiga kura
nchini kwa wananchi wote, ikiwa ni sehemu ya mchakato wa kuboresha Daftari la
Kudumu la Wapigakura na ungetekelezwa Septemba mwaka huu, kwa kugharimu Sh
bilioni 293.
Awali, akitoa taarifa ya uboreshaji wa daftari hilo, Makamu Mwenyekiti wa
Tume hiyo ambaye ni Jaji Mkuu mstaafu wa Zanzibar, Hamid Mohamoud Hamid alisema
NEC wanaamini watapokea fedha zaidi wakati wanaendelea na uboreshaji huo.
Alisema uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapigakura, ungeanza Septemba
mwaka huu lakini haikuwezekana, kutokana na kuchelewa kupatikana kwa fedha
kutoka serikalini.
Alisema katika uboreshaji huo, tume imepanga kufanya majaribio ya uboreshaji
wa daftari kwa kutumia mfumo mpya wa ‘Biometric Voter Registration’ (BVR)
katika majimbo matatu ya uchaguzi nchini, ambayo ni Kawe Manispaa ya Kinondoni
jijini Dar es Salaam, Kilombero katika Halmashauri ya Mji wa Kilombero na Mlele
katika mkoa wa Katavi.
“Kulingana na ratiba ambayo Tume imejipangia, majaribio ya uboreshaji wa
daftari yataanza kufanyika katikati ya Novemba mwaka huu na tayari Tume
imekwishapokea baadhi ya vifaa muhimu vya uandikishaji ikiwemo Fomu za
Uandikishaji na sasa kinachosubiriwa ni kupokea BVR Kits (vifaa) 250 wakati
wowote kuanzia leo,” alisema.
Hamid alisema baada ya majaribio kukamilika, itafuatiwa na uboreshaji wa
jumla katika maeneo mengine kwa wakati mmoja katika mikoa yote, isipokuwa mkoa
wa Dar es Salaam na Zanzibar, ambayo uandikishaji utafanyika baada ya mikoa
mingine kukamilika.
Alisema muda wa uandikishaji ni siku saba katika kila kituo na uandikishaji
umepangwa kufanyika mwanzoni mwa Januari mwakani hadi katikati ya Februari
mwakani katika mikoa yote, isipokuwa Dar es Salaam na Zanzibar, ambapo
uboreshaji utafanyika mwishoni mwa Februari mwakani.
Akizungumzia suala la muda wa kura za maoni, alisema kwa sasa wanajikita
katika uboreshaji wa daftari kutokana na kuwa tume hiyo, ilishauri serikali kwa
sasa daftari la wapigakura kuwa lina kasoro na ingebidi kuboreshwa, kabla ya
kufanyika kwa kura ya maoni ya Katiba pendekezwa.
“Tulishauri kuwa ni vyema kura hiyo ingepigwa baada ya kukamilika kwa
Daftari, hivyo tunategemea kura hiyo ya maoni itafanyika muda wowote baada ya
kukamilika kwa uboreshaji ili haki itendeke,” alisisitiza.
Mbowe wa Chadema ang’aka
Hata hivyo, Mwenyekiti wa Taifa wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo
(Chadema), Freeman Mbowe amesema NEC haijashirikisha vyama vya siasa kwenye
mchakato wa kuboresha Daftari la Wapigakura, jambo ambalo linatia shaka
utekelezaji wake.
Mbowe alisema vyama vya siasa havijashirikishwa kama wadau kwenye mchakato
huo na kwamba taarifa hiyo ya NEC, ndio wanaisikia kutoka kwa vyombo vya habari
na kwamba hawana taarifa rasmi.
“Tume haijatushirikisha na jambo hili ni la wadau wote na vyama vya siasa ni
wadau wakubwa wa suala hili, sasa kama hatushirikishwi tunasikia tu kutoka
kwenu, kwa kweli haya ndio mambo yanayoleta malumbano,” alisema Mbowe
alipohojiwa na gazeti hili jana.
Alisema Tume ya Uchaguzi inavyoonekana inawasiliana na chama kimoja cha CCM
na kuviacha vyama vingine, wakati mchakato wa uboreshaji Daftari la Wapigakura
ni suala la umma, linalopaswa vyama vyote kushirikishwa.
“Uchaguzi huru na haki unaanzia mapema wakati wa uboreshaji wa Daftari la
Wapigakura, lakini cha ajabu vyama vya siasa hatushirikishwi kama wadau kutoa
mawazo yetu na kisha ndio Tume itangaze kwa vyombo vya habari,” alisisitiza
Mbowe.
Kuhusu fedha ambazo NEC wamepata hadi sasa ni Sh bilioni 15, na mahitaji
halisi ya uboreshaji daftari hilo ni Sh bilioni 293, Mbowe alisema fedha
zilizopatikana ni chache na haziwezi kutosha kufanya utekelezaji. Alisema
hawajui Tume ina uhakika gani, kama fedha zinazohitajika, zitapatikana kwa
wakati.
Maoni
Chapisha Maoni