CHUJI NA MOMBEKI WAAMBULIA PATUPU OMAN, WAAMUA KURUDI DAR, JERRY SANTO AAMUA KUKOMAA UARABUNI.

Mambo magumu; Kiungo Athumani Iddi 'Chuji' anarudi nyumbani baada ya kukwama Oman
WACHEZAJI wawili wa Tanzania waliokwenda Oman kucheza soka ya kulipwa, kiungo Athumani Iddi ‘Chuji’ na mshambuliaji Betram Mombeki wamekwama na wanarejea nyumbani leo.

Wachezaji hao waliitwa na Oman Club kwa ajili ya kusaini mikataba, lakini walipofika huko wakakutana na kikwazo cha kocha ambaye alikuwa tayari ana wachezaji aliotaka wasajiliwe.

“Kocha alikuwa ana wachezaji wake, sasa hakutaka hata kuwafuatilia akina Chuji ambao waliletwa na viongozi.

Mwisho wa siku viongozi ikabidi wakubali matakwa ya kocha, kwa hiyo vijana wapo kwenye ndege (Oman Air) tayari wanarudi nyumbani,”kimesema chanzo kutoka Oman.

Hata hivyo, kiungo wa zamani wa Simba SC na Coastal Union, Mkenya Jerry Santo aliyekwenda sambamba na wawili hao, yeye ameamua kubaki akitafutiwa timu nyingine na wakala Mtanzania anayeishi huko, Said Maaskary.

“Santo na akina Chuji wote walikutana na wakala mmoja Mtanzania anayeishi huku, Maaskary. Akazungumza nao wabaki awatafutie timu, lakini wao wakasema wanarudi tu nyumbani,”kimeongeza chanzo hicho. 

Wakati Chuji alikwenda Oman baada ya kumaliza Mkataba wake Yanga SC, Mombeki naye alikwenda huko baada ya kuondoka Simba SC kufuatia kutofautiana na aliyekuwa kocha wa klabu hiyo, Mcroatia, Zdravko Logarusic.

Tayari Logarusic ameondolewa Simba SC na nafasi yake amechukua Mzambia, Patrick Phiri. 

Oman Club ambayo kwa Oman inafahamika kama Al-Ahmar, au ‘Wekundu’, maskani yake ni Jiji la Muscat na kwa sasa inacheza Ligi Daraja la Kwanza, ikitumia Uwanja wa Sultan Qaboos Sports Complex, ingawa pia hutumia Uwanja wa Royal Oman Police kwa mechi zake za nyumbani. 

Viwanja vyote vinamilikiwa na Serikali, lakini Oman Club pia wanamiliki Uwanja wao wenye vifaa vyote ambao huutumia kwa mazoezi pekee.

Maoni