Mawaziri, wabunge kutimuliwa kwenye nyumba TBA Dodoma.

Wakala wa Majengo Tanzania (TBA) imefanya uamuzi mgumu wa kuwatimua baadhi ya wapangaji wa nyumba zake zilizopo mjini Dodoma ambao ni wadaiwa sugu, wakiwamo mawaziri saba na wabunge 15.
 
TBA katika kutekeleza uamuzi huo imekabidhi Kampuni ya Yono Action Mart orodha ya majina ya watu hao wanaodaiwa kiasi cha Sh800 milioni, ili waondolewe kwa nguvu kwenye nyumba hizo wanazoishi.
Akizungumza na Mwananchi juzi Mkurugenzi Mtendaji wa TBA, Elius Mwakalinga, alithibitisha kuwa ofisi yake inachukua hatua hiyo kwa mujibu wa sheria kwa sababu wapangaji hao wamekwenda kinyume na mikataba yao.
“ Hatukupenda kuchukua hatua hii, lakini ukweli ni kwamba madeni hayo ni ya muda mrefu, kazi tunayofanya ni kwa manufaa ya maendeleo ya nchi na siyo yetu binafsi, hivyo tulitegemea wangetimiza wajibu wao wa kulipa lakini imekuwa kinyume,” alisema Mwakalinga.
Alisema fedha ambazo TBA inadai hadi sasa zimefikia jumla ya Sh 800 milioni ambazo kama zingekuwa zimelipwa zingewasaidia kutimiza wajibu wao wa kujenga baadhi ya nyumba mpya au kukarabati zile zinazotakiwa kufanyiwa hivyo.
“Walipewa notisi na ofisi yetu kule Dodoma baadhi yao waliitikia wito kwa kulipa madeni yao, wakiwamo hata maofisa wa Ikulu, walitoa ushirikiano mzuri, nafikiri kwa kutambua wajibu tulio nao TBA,” alisema.
Mwakalinga alisema kuwa TBA imeona iwahusishe kampuni ya udalali ya Yono Action Mart kwa sababu wao wana majukumu mengi ya ujenzi wa nyumba mpya za watumishi wa Serikali.
“ Gharama za kumlipa dalali huyo, watatakiwa kulipa hao hao wanaodaiwa kwa mujibu wa sheria, sisi hatuna bajeti hiyo,” alisema Mwakalinga ambaye alikataa kuwataja wadaiwa hao akieleza kuwa jukumu hilo tayari lipo kwa Yono.
Mkurugenzi wa Yono Action Mart, Yono Kevela, kwa upande wake alisema baada ya kupokea kazi hiyo, walitoa notisi ya siku 14 kwa wahusika ili kuwapa nafasi ya kulipa madeni yao.
“ Wale ambao wamelipa kutokana na ile notisi wamejinusuru, lakini wale ambao hawajalipa kwa kweli nimetuma kikosi kazi changu ambacho ninakiamini, kwamba hakina woga katika kutimiza majukumu tuliyopewa, natarajia kesho wataanza kazi, hiyo,” alisema Kevela. 

Baadhi ya mawaziri waliotajwa kwenye orodha hiyo ni Waziri wa Viwanda na Biashara Dk Abdallah Kigoda, anayedaiwa Sh7.5 milioni, ambaye alipohojiwa na gazeti hili kwa njia ya simu kuhusu deni hilo alisema: “Mimi sina habari hiyo nipo Nairobi, Kenya,”.
Mwingine ni Waziri wa Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu anayedaiwa Sh 9.4 milioni, ambaye aliliambia gazeti hili kuwa ana taarifa ya deni hilo, lakini kwa wadhifa wake hawajibiki binafsi.
“ Nakumbuka niliona barua, lakini kwa utaratibu ninaoujua ni kwamba mawaziri wote hatujigharamii kwa hilo , bali tunalipiwa na Serikali sasa nafikiri labda wizara ilijisahau, nakuhakikishia binafsi siwajibiki,” alisema Nyalandu.

Maoni